Wachezaji John Boko na Salumu Aboubakar wakigeuka watazamaji wakati wenzao wakifanya mazoezi huko Kigali leo.
KIUNGO Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na
mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ wameshindwa kufanya mazoezi na timu
yao leo, Azam FC kutokana na kusumbuliwa na maumivu.
Azam baada ya kushinda mechi ya kwanza
katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame jana mabao 4-0
dhidi ya KMKM ya Zanzibar, leo imeendelea na mazoezi mjini hapa.
Wakati wachezaji wote wakifanya
mazoezi Uwanja wa Kiyovu, eneo la Nyamirambo mjini hapa, Sure Boy na Bocco walikuwa
nje wakiugulia maumivu yao.
Sure Boy anasumbuliwa na maumivu ya
mguu aliyoyapata jana katika mechi ya pili ya Kundi B na KMKM Uwanja wa
Amahoro, wakati Bocco aliumia chini ya goti.
Kocha Joseph Marius Omog, raia wa
Cameroon aliamua kuwapumzisha wachezaji hao ili wapate ahueni wakati timu
ikijiandaa na mchezo wa tatu wa kundi lake dhidi ya Atlabara ya Sudan Kusini
kesho.
“Si maumivu makubwa sana, nadhani
baada ya mapumziko ya leo kesho wanaweza kuwa fiti, lakini naangalia uwezekano
wa kuwapumzisha zaidi,”alisema Omog.
Azam FC imevuna pointi nne katika
mechi mbili baada ya sare ya bila kufungana katika mchezo wa kwanza dhidi ya
Rayon Sport na sasa inaongoza Kundi A, ikifuatiwa na wenyeji hao wenye pointi
nne pia, KMKM na Atlabara zina pointi moja kila moja, wakati Adamma City ya
Ethiopia haina kitu.
Azam FC itakuwa imejihakikishia
kwenda Robo Fainali ya michuano ya mwaka huu iwapo itashinda mchezo wa kesho
dhidi ya timu hiyo ya Sudan Kusini.
Kocha Omog amesema wachezaji wengine
wote wako fiti kuelekea mchezo huo na ana matumaini ya kufanya vizuri.
Mkule.bogsport.com
No comments:
Post a Comment