Miongoni mwa msafara wa Azam fc wakiwa uwanja wa ndege tayari kwa safari.
Kikosi cha cha wachezaji 20 wa Azam
FC kimeondoka jioni ya leo Dar es Salaam kwenda Kigali, Rwanda kushiriki Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame michuano inayoanza wikiendi
hii mjini Kigali, Rwanda.
Azam FC imechukua nafasi ya Yanga SC
iliyoenguliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa
kushindwa kuthibitisha kupeleka kikosi cha kwanza pamoja na kocha Mkuu, Marcio
Maximo kwa mujibu wa kanuni za mashindano.
Yanga SC ilitakiwa hadi juzi jioni
kuwa imethibitisha na kutuma kikosi, lakini haikufanya hivyo na CECAFA
ikawasiliana na TFF kuwaambia wapeleke timu nyingine iliyo tayari na zali
likawaangukia Azam FC.
Yanga SC ilitaka kupeleka kikosi cha
vijana kwenye nashindano hayo, jambo ambalo CECAFA waliwakatalia wakiwaambia
hiyo si michuano ya watoto.
Kikosi cha Azam kilichoondoka chini
ya kocha Joseph Marius Omog raia wa Cameroon ni makipa; Aishi Manula, Mwadini
Ally, mabeki Waziri Salum, Gadiel Michael, Shomary Kapombe, Abdallah Kheri,
Aggrey Morris, Said Mourad na David Mwantika.
Viungo Kipre Balou kutoka Ivory
Coast, Salum Abubakar, Mudathir Yahya, Himid Mao, Khamis Mcha ‘Vialli’, Farid
Mussa na Joseph Peterson wa Haiti, wakati washambuliaji ni Mrundi Didier
Kavumbangu, Leonel Saint- Preux wa Haiti, Kipre Herman Tchetche wa Ivory Coast
na John Bocco ‘Adebayor’.
Azam FC, mabingwa wa Tanzania Bara,
sasa wanaingia Kundi A katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Kagame ya 40 pamoja na wenyeji, Rayon Sport, Coffee ya Ethiopia, Atlabara ya
Sudan Kusini na KMKM ya Zanzibar.
Kundi B lina timu za APR ya Rwanda,
KCC ya Uganda, Flambeau de L’Est ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya na Telecom ya
Djibouti wakati Kundi C linaongozwa na mabingwa watetezi, Vital’O ya Burundi,
El Merreikh ya Sudan, Polisi ya Rwanda na Benadir ya Somalia.
Timu 14 zinatarajiwa kushiriki
michuano hiyo kuanzia Agosti 8 hadi 24 mwaka huu- jumla ya mechi 34 zikichezwa
katika viwanja vya Amahoro na Nyamirambo, Kigali.
Azam itacheza mechi ya kwanza kesho
jioni dhidi ya wenyeji Rayon Sport Uwanja wa Amahoro, baada ya
KMKM ya Zanzibar na Atlabara ya
Sudan Kusini kumenyana katika mechi ya ufunguzi mchana.
Azam FC itarudi tena dimbani, Agosti
10 kumenyana na jirani zao KMKM, kabla ya kucheza na Atlabara Agosti 12 na
kukamilisha mechi za kundi lake, kwa kumenyana na Adamma ya Ethiopia Agosti 16.
Mkule.blogsport.com
No comments:
Post a Comment