Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho
Kikwete- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dk. Fennela Mukangara-
Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Ndugu Dioniz Malinzi- Mwenyekiti wa
Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
Mkuu wa msafara wa FIFA/Coca-Cola
Bw Yebeltal Getachew- Meneja Mkazi
wa Coca-Cola
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF
Wageni waalikwa
Mabibi na mabwana
Mheshimiwa Rais, nianze kwa
kukushukuru kwa heshima uliyoupatia mpira wa Tanzania kwa kukubali kuwa mgeni
rasmi katika hafla yetu hii ya kupokea Kombe halisi la Dunia.
Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania
kupewa heshima hii na FIFA na washirika wake kampuni ya vinywaji ya Coca-Cola.
Coca-Cola ni washirika wetu wa
karibu na wamekuwa wakidhamini mashindano ya kitaifa ya vijana tangu
mwaka 2007, mashindano ambayo kwa
kiasi kikubwa yamesaidia kuibua vipaji vingi ambapo baadhi yao wameweza
kuchezea timu zetu za Taifa na klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza.
Tunawashukuru sana Coca-Cola na
tunaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano katika jitihada zao za kuendeleza
soka ya vijana.
Mheshimiwa Rais, tarehe 19 Novemba,
2009 wakati unapokea kombe hili hili hapa Tanzania ulitoa changamoto kadhaa kwa
uongozi wa mpira wa Tanzania.
Ulitushauri tuimarishe uongozi na
utendaji wetu kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya hadi klabu, ulitushauri
tupate walimu wenye uzoefu wa kutosha kufundisha timu zetu za mpira na pia
ulitushauri tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji toka
wakiwa na umri mdogo.
Mheshimiwa Rais ushauri wako kwetu
tuliuzingatia na tulifanya jitihada za kuufanyia kazi. Hali ya utulivu katika
uendeshaji mpira wetu imeimarishwa na pale palipoonyesha dalili za migogoro
tulikemea na ikibidi tulichukua hatua madhubuti kutatua migogoro.
Tumefanya kozi mbalimbali za
kuwaendeleza walimu wetu wa mpira, waamuzi, madaktari na viongozi
wetu wa ngazi mbalimbali na matokeo yake yanaonekana katika kuinuka kwa viwango
vyao vya ufundishaji na utoaji uamuzi uwanjani.
Mheshimiwa Rais kama ulivyotuelekeza
mwaka 2009 maendeleo ya soka ya vijana ndio ufunguo wa maendeleo ya mpira kwa
Taifa letu. Uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani alfajiri ya tarehe 28,
Oktoba 2013 tayari unalifanyia kazi jambo hili kwa umakini mkubwa.
Uongozi wetu umeamua kuwa ufunguo wa
mpango endelevu wa soka ya vijana utakuwa ni Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali
za Afrika za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.
Fainali hizi uhusisha mataifa manane
yanayogawanywa katika makundi mawili ya awali akiwemo mwenyeji ambaye anaingia
moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya fainali hizi. Aidha timu mbili
zinazoongoza makundi haya mawili moja kwa moja huwa zinacheza fainali za dunia
za vijana chini ya umri wa miaka
17.
Fainali hizi ndizo ziliwaibua akina
Luis Figo, Ronaldino, Nwankwo Kanu, Michael Essien, Nii Lamptey, Celestine
Babayaro na wengine kadhaa.
Ili tupate timu nzuri ya vijana umri
chini ya miaka 17 mwaka 2019 itabidi mwaka kesho 2014 tufanye mashindano ya kitaifa ya vijana chini ya umri wa chini wa miaka 12 ili tupate
kikosi cha kwanza cha Taifa U-12, kikosi ambacho kitakuwa pamoja kuelekea 2019.
Katika kuboresha kikosi hiki mwaka
2015 tutafanya mashindano ya kitaifa ya umri chini ya miaka 13, 2016 yatakuwa
ya umri chini ya miaka 14, 2017 yatakuwa ya umri chini ya miaka 15 na 2018
yatakuwa ya umri chini ya miaka 16 na ambayo yatatupatia kikosi cha mwisho cha
kuingia nacho fainali za vijana mwaka 2019.
Tunaamini timu nzuri za Taifa U-17
ya mwaka 2019 itatuzalishia kikosi imara kitakachoshiriki Olimpiki za 2020,
kucheza CHAN na AFCON zitakazofuata na hatimae kufaulu fainali za dunia 2026
ambayo ni miaka kumi na tatu kuanzia sasa.
Ninashukuru tarehe 21 Novemba 2013,
Shirikisho la mpira barani Afrika (CAF) liliniteua kuwa Mjumbe wa Kamati ya
Maandalizi ya michuano ya Afrika umri
chini ya miaka 17 (CAF U-17 Organizing
Committee), tunaamini kuwepo kwangu katika kamati hii muhimu ya CAF kutasaidia
Tanzania ipate wenyeji huu mwaka 2019.
Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa kanuni
za CAF nchi inayoomba uenyeji wa fainali za michuano ya Afrika haina budi
ionyeshe barua ya kuungwa mkono na nchi yake(Letter of support from
Government).
Wiki ijayo tutawasilisha barua
kwenye Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya kuomba kuungwa mkono
na Serikali katika azma yetu hii, tunaomba Serikali ituunge mkono katika jambo
hili.
Mheshimiwa Rais nimalizie kwa
kukushukuru tena kwa uwepo wako katika shughuli hii muhimu, ninaishukuru Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano wanaotupa katika
shughuli zetu za kila siku, FIFA nawashukuru sana kwa kutuwezesha kuwa moja ya
nchi 88 duniani zilizopokea kombe hili, Coca-Cola asanteni sana tuzidi kuwa
karibu.
Watanzania wenzangu ninaomba tuje
kwa wingi kesho Jumamosi kutembelea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuliona
Kombe hili na kupiga nalo picha. Imani yangu ni kuwa ipo siku Kapteni wa Timu
yetu ya Taifa atamkabidhi Rais wa Tanzania kombe hili.
Asante
No comments:
Post a Comment