Pages

Ads 468x60px

Saturday, November 30, 2013

SALAMU ZA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA KWENYE HAFLA YA KUPOKEA KOMBE HALISI LA DUNIA TANZANIA





Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Dk. Fennela Mukangara- Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo

Ndugu Dioniz Malinzi- Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT)

Mkuu wa msafara wa FIFA/Coca-Cola

Bw Yebeltal Getachew- Meneja Mkazi wa Coca-Cola

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF

Wageni waalikwa

Mabibi na mabwana

Mheshimiwa Rais, nianze kwa kukushukuru kwa heshima uliyoupatia mpira wa Tanzania kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla yetu hii ya kupokea Kombe halisi la Dunia.

Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kupewa heshima hii na FIFA na washirika wake kampuni ya vinywaji ya Coca-Cola.

Coca-Cola ni washirika wetu wa karibu na wamekuwa wakidhamini mashindano ya kitaifa ya vijana tangu
mwaka 2007, mashindano ambayo kwa kiasi kikubwa yamesaidia kuibua vipaji vingi ambapo baadhi yao wameweza kuchezea timu zetu za Taifa na klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza.

Tunawashukuru sana Coca-Cola na tunaahidi  kuendelea kuwapa ushirikiano katika jitihada zao za kuendeleza soka ya vijana.

Mheshimiwa Rais, tarehe 19 Novemba, 2009 wakati unapokea kombe hili hili hapa Tanzania ulitoa changamoto kadhaa kwa uongozi wa mpira wa Tanzania.

Ulitushauri tuimarishe uongozi na utendaji wetu kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya hadi klabu, ulitushauri tupate walimu wenye uzoefu wa kutosha kufundisha timu zetu za mpira na pia ulitushauri tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji toka wakiwa na umri mdogo.

Mheshimiwa Rais ushauri wako kwetu tuliuzingatia na tulifanya jitihada za kuufanyia kazi. Hali ya utulivu katika uendeshaji mpira wetu imeimarishwa na pale palipoonyesha dalili za migogoro tulikemea na ikibidi tulichukua hatua madhubuti kutatua migogoro.

Tumefanya kozi mbalimbali za kuwaendeleza walimu wetu wa mpira, waamuzi, madaktari na viongozi wetu wa ngazi mbalimbali na matokeo yake yanaonekana katika kuinuka kwa viwango vyao vya ufundishaji na utoaji uamuzi uwanjani.

Mheshimiwa Rais kama ulivyotuelekeza mwaka 2009 maendeleo ya soka ya vijana ndio ufunguo wa maendeleo ya mpira kwa Taifa letu. Uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani alfajiri ya tarehe 28, Oktoba 2013 tayari unalifanyia kazi jambo hili kwa umakini mkubwa.

Uongozi wetu umeamua kuwa ufunguo wa mpango endelevu wa soka ya vijana utakuwa ni Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Afrika za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.

Fainali hizi uhusisha mataifa manane yanayogawanywa katika makundi mawili ya awali akiwemo mwenyeji ambaye anaingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya fainali hizi. Aidha timu mbili zinazoongoza makundi haya mawili moja kwa moja huwa zinacheza fainali za dunia za vijana chini ya umri wa miaka
17.

Fainali hizi ndizo ziliwaibua akina Luis Figo, Ronaldino, Nwankwo Kanu, Michael Essien, Nii Lamptey, Celestine Babayaro na wengine kadhaa.

Ili tupate timu nzuri ya vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019 itabidi mwaka kesho 2014 tufanye mashindano ya kitaifa ya vijana chini ya umri wa chini wa miaka 12 ili tupate kikosi cha kwanza cha Taifa U-12, kikosi ambacho kitakuwa pamoja kuelekea 2019.

Katika kuboresha kikosi hiki mwaka 2015 tutafanya mashindano ya kitaifa ya umri chini ya miaka 13, 2016 yatakuwa ya umri chini ya miaka 14, 2017 yatakuwa ya umri chini ya miaka 15 na 2018 yatakuwa ya umri chini ya miaka 16 na ambayo yatatupatia kikosi cha mwisho cha kuingia nacho fainali za vijana mwaka 2019.

Tunaamini timu nzuri za Taifa U-17 ya mwaka 2019 itatuzalishia kikosi imara kitakachoshiriki Olimpiki za 2020, kucheza CHAN na AFCON zitakazofuata na hatimae kufaulu fainali za dunia 2026 ambayo ni miaka kumi na tatu kuanzia sasa.

Ninashukuru tarehe 21 Novemba 2013, Shirikisho la mpira barani Afrika (CAF) liliniteua kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya michuano ya Afrika umri
chini ya miaka 17 (CAF U-17 Organizing Committee), tunaamini kuwepo kwangu katika kamati hii muhimu ya CAF kutasaidia Tanzania ipate wenyeji huu mwaka 2019.

Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa kanuni za CAF nchi inayoomba uenyeji wa fainali za michuano ya Afrika haina budi ionyeshe barua ya kuungwa mkono na nchi yake(Letter of support from Government).

Wiki ijayo tutawasilisha barua kwenye Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya kuomba kuungwa mkono na Serikali katika azma yetu hii, tunaomba Serikali ituunge mkono katika jambo hili.

Mheshimiwa Rais nimalizie kwa kukushukuru tena kwa uwepo wako katika shughuli hii muhimu, ninaishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano wanaotupa katika shughuli zetu za kila siku, FIFA nawashukuru sana kwa kutuwezesha kuwa moja ya nchi 88 duniani zilizopokea kombe hili, Coca-Cola asanteni sana tuzidi kuwa karibu.

Watanzania wenzangu ninaomba tuje kwa wingi kesho Jumamosi kutembelea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuliona Kombe hili na kupiga nalo picha. Imani yangu ni kuwa ipo siku Kapteni wa Timu yetu ya Taifa atamkabidhi Rais wa Tanzania kombe hili.

Asante

AZAM FC YAMTAMBULISHA KOCHA WAKE MPYA ALIYECHUKUA MIKOBA YA STEWART HALL.

Klabu ya Azam inapenda kuufahamisha umma hususan wapenzi wa mpira wa miguu kuwa imeingia mkataba na kocha Joseph Marius Omograia wa Cameroon kwa kipindi cha miakamiwili (2) kuanzia leo.
Kocha Omog ni bingwa kwani anakuja kuifundisha Azam akiwa ametoka kuiongoza klabu ya A.C Leopards ya Jamhuri ya Kongo (Brazaville) kutwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo kwa misimu miwili mfululizo (2012 na 2013). Timu hii ilikuwa haijatwaa ubingwa wa ligi kwa zaidi ya miaka 30. Kwa mwaka huu wametwaa ubingwa wakiwaacha wapinzani wao, Diables Noirs kwa pengo la pointi kumi (10) wakikusanya pointi 87 katika ligi yenye timu 18.  
Pia ni mwaka jana tu (2012) aliiwezesha A.C Leopards kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwa kuzipiga kumbo timu ngumu na zenye uzoefu mkubwa kama vile Mas de Fes ya Morocco, Heartlands ya Nigeria na Sfaxien ya Tunisia.   
Mafanikio hayo ya kutwaa ubingwa wa Afrika yalifikiwa baada ya miaka 38 tangu klabu ya Jamhuri yas Kongo ifanye hivyo, na kumfanya kocha Omog kuwa moja ya makocha wa kupigiwa mfano barani Afrika.
Kadhalika mwaka huu 2013, A.C Leopards chini ya ukufunzi wa Omog ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya mabnigwa Afrika na kupangwa katika kundi moja na timu mbili zilizocheza fainali; Al Ahly ya Misiri (bingwa) na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Yote hayo ameyafanya akitumia asilimia kubwa ya wachezaji wa ndani ya Kongo huku akiwainua kutoka katika hali ya kuonekana wachezaji wa wastani hadi kuwa tishio na kuhofiwa kote barani Afrika.
Azam Football Club inamuona kocha Omog kuwa anakidhi vigezo vya kuendana na dira ya klabu ambayo ni kukuza na kuwaendeleza wachezaji na kushindana kwa kiwango cha juu kwa lengo la kuwa mabingwa katika mashindano mabalimbali ambayo timu inashiriki.
Uongozi wa Azam FC utampatia ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha malengo na mipango thabiti ya klabu.
 
Maelezo Binafsi
 

Kocha Omog ni mchezaji wa zamani wa timu ya Dragon Yaounde Cameroon. Alipata mafunzo ya ualimu wa michezo na elimu ya viungo (Sports and physical education)  kutoka chuo cha vijana na michezo (Higher Institute of Youth and Sports, INJS Yaounde).
Baadaye alipata fursa ya kujiendeleza nchini Ujerumani ambako mwaka 1987 alitunukiwa stashahada ya ukufunzi wa mpira wa miguu na leseni B ya ukocha kwa viwango vya Shirikisho la mpira wa miguu barani Ulaya, UEFA.
Aliporejea nyumbani kwao Cameroon Joseph Marius Omog, alifundisha kabumbu katika klabu mbalimbali, zikiwemo; Fovu of Baham na Aigle of Menoua na kufanikiwa kufuzu kwa fainali za kombe la Cameroon. Mwaka 2001 aliteuliwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Cameroon, Indomitable Lions chini ya kocha raia wa Ujerumani Winfried Schafer.
Omog amewahi pia kufundisha timu ya taifa ya Cameroon iliyoundwa na wachezaji wa ndani ijulikanayo kama Intermediate Lions hadi mwaka 2010 na baada ya hapo akelekea Kongo kuionoa A.C Leopards kwa mafanikio makubwa na hasa kutwaa ubingwa wa kombe la Shirikisho wakiifunga Djoliba ya Mali kwa ushindi wa jumla wa magoli 4-3 katika michezo miwili ya fainali.
Uongozi,                                                                            
Azam Football Club,
Novemba 30, 2013

Thursday, November 28, 2013

UGANDA YAENDELEA KUZIBURUZA NCHI WANACHAMA WA CECAFA KATIKA MSIMAMO WA UBORA WA SOKA DUNIANI




Tanzania imepanda kwenye msimamo wa ubora wa soka duniani kwatakwimu zilizotolewa leo na shirikisho la soka duniani Fifa.
Takwimu hizo ambazo hutolewa kila mwezi Tanzania ipanda kwa nafasi tano kutoka nafasi ya 129 mwezi uliopita hadi katika nafasi ya 124 mwezi huu.

Katika takwimu hizo Uganda imeendelea kushika nafasi ya kwanza  kwa nchi wanachama wa Cecafa kwakuwa nafasi ya 86 kidunia huku Ethiopia ikishika nafasi ya pili kwa ukanda huo huku kidunia ikiwa nafasi ya 93.

Burundi ya 112 kidunia kwaukanda Cecafa inashika nafasi ya tatu,Kenya ya 4 kwa ukanda huo ikiwa nafasi ya 117 kidunia huku nafasi ya 5 kwa ukanda wa Cecafa ikishikwa na Tanzania iliyopo nafasi ya 124 kidunia.
Rwanda inashika nafasi ya 6 kwa ukanda wa Cecafa ikiwa nafasi ya 127 kidunia,Sudani inashika nafasi ya 7 kwa Cecafa huku ikishika nafasi ya 130 kwa dunia.

Katika msimamo huo wa ubora wa soka duniani Eritrea inashika nafasi ya 8 kwa nchi wanachama wa Cecafa kidunia ikishika nafasi ya 199,Sudan Kusini inashika nafasi ya 9 kwa ukanda wa Cecafa wakati kidunia ikishika nafasi ya 201.

Somalia ndiyo inayoburuza mkia kwenye takwimu hizo za obora wa soka duniani kwa nchi wanachama wa Cecafa ikishika nafasi ya 10 huku kidunia ikishika nafasi ya 204.

mkule.blogspot.com

IVO AIONGOZA KILI STARS KWENYE SARE NA CHIPOLOPOLO KATIKA MICHUANO YA CHALLANGE.






Timu ya taifa ya Tanzania bara Kilimanjaro stars leo imetoka sare ya kufungana goli 1 kwa 1 na timu ya taifa ya Zambia Chipolopolo kwenye mashindano ya kombe la Challenge yaliyoanza jana nchini Kenya.
Katika pambano hilo Zambia ndiyo iliyokuwa yakwanza kupata goli kupitia kwa mchezaji Ronald Kampamba  Dkk ya 41  Kabla ya Kili stars kusawazisha kunako dkk ya 48 likifungwa kwa kichwa na Said Morad.
Baada ya mchezo kumalizika kocha mkuu wa Kilimanjaro Stars Kim Poulsen amesema ameridhika na uwezo wa kikosi chake hivyo anamatumaini ya kufanya vyema michezo inayofuata.
Kim pia amesema wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaoichezea TP Mazembe ya DRC Congo watakuwepo katika michezo inayofuata baada yah ii leo kukosekana kwenye kikosi hicho.
Naye kocha mkuu wa Chipolopolo mfaransa Patrice Beaumelle amezipongeza timu zote kwakucheza soka safi  huku akieleza matarajio yake kwenye michezo inayofuata kwakusema matokeo waliyoyapata ni mwanzo mzuri hivyo hanashaka yeyote na michezo inayofuata.
Kwaupande wake kiungo Salum Aboubakary wa Kili stars ambaye alichaguliwa nyota wa mchezo amesema kikosi chao kimecheza vibaya ungwe ya kwanza lakini kipindi cha pili walibadilika na hatimae kusawazisha goli na hatimae kupata sare hiyo.
Pia kiungo huyo ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya taifa ya Tanzania Aboubakari Salumu “sure boy amelalamikia uwanja  wa Kenyatta uliopo Machakosi walioutumia leo kuwa haukua mzuri hasa baada ya mvua kunyesha.

Kwa matokeo hayo, Burundi inaongoza kundi hilo baada ya kuifunga Somalia 2-0 katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo.
Kikosi cha Stars kilikuwa; Ivo Mapunda, Himid Mao, Erasto Nyoni, Said Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk89, Hassan Dilunga/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk85, Elias Maguri/Haroun Chanongo dk72, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.

Chipolopolo; Nsabata Toaster, Bronson Chama, Jimmy Chisenga/Kabaso Chongo dk67, Christopher Munthali, Rodrcik Kabwe, Stanley Nshimbi/Alex Nshimbi dk57, Sydney Kalume, Kondwani Mtonga, Felix Katongo/Salulani Phiri dk73, Ronald Kampamba na Festus Ndewe.  

Kwenye mchezo wa awali hii leo Burundi ilifanikiwa kuifunga Somalia magoli 2 kwa 0

Kesho ni zamu ya Sudan na Eritrea kwenye uwanja wa Kenyata uliopo Machakosi majira ya saa nane kamili mchana wakati mabingwa watetezi Uganda wataikabili Rwanda kwenye uwanja huohuo wa Kenyatta saa kumi jioni.

mkule.blogspot.com