Pages

Ads 468x60px

Sunday, December 29, 2013

KLABU ZATAKIWA KUREKEBISHA KASORO USAJILI MDOGO.



  

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili mambo mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo usajili wa dirisha dogo ambapo klabu zenye matatizo zimepewa hadi Januari 10 mwakani kurekebisha.

Baadhi ya klabu ikiwemo Simba zimezidisha idadi ya wachezaji, hivyo zimepewa hadi muda huo kupunguza ambapo zikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati yenyewe.

Simba ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo lakini imewasilisha majina ya wachezaji sita.

Pia klabu nyingine zimetakiwa ama kuvunja mikataba ya wachezaji au kuendelea kuwa nao, na si kuendelea kuwalipa mishahara wakati imeshawaondoa katika orodha yao.

RAGE BADO MWENYEKITI HALALI SIMBA
Ismail Aden Rage ndiye Mwenyekiti halali wa Simba ambapo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imemtaka kuitisha Mkutano Mkuu kwa mujibu wa taratibu za klabu ya Simba.

Kamati imebaini upungufu kadhaa wa kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba 18, 2013 kwa kumsimamisha Mwenyekiti wao. Upungufu huo ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.

Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.

Hivyo, agizo za Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe mkutano lipo palepale. Pia Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.

Katika mkutano huo wa kujaza nafasi, ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya Geofrey Nyange aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.

TFF inakumbusha wanachama wake wote (vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba zao. Kamati pia imegundua ukikwaji wa maadili katika suala hili, hivyo, litapelekwa katika kamati husika.

Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.

Kuhusu mchezaji Emmanuel Okwi ambaye aliuzwa nchini Tunisia, TFF inafahamu kuwa klabu ya Simba bado haijalipwa na itasaidia kufuatilia FIFA fedha za mauzo ya mchezaji huyo.

AJENDA, MUHTASARI WA KUMNG’OA KATIBU COREFA ZATAKIWA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kuwasilisha ajenda na muhtasari wa vikao vilivyofanya uamuzi wa kumvua madaraka Katibu wake Riziki Majalla.

Ajenda na muhtasari unaotakiwa ni wa vikao vya Kamati ya Utendaji iliyomsimamisha Katibu huyo kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi yake, na Mkutano Mkuu ambao ulimvua madaraka.

WATAKIWA KUHESHIMU UAMUZI WA TPLB
Wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wametakiwa kuheshimu uamuzi halali unaofanywa na vyombo vyake kwa kuzingatia katiba na kanuni zake.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imetoa maelekezo hayo baada ya klabu ya Stand United kukata rufani kupinga uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuagiza mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Kanembwa JKT iliyovunjika kurudiwa Februari Mosi mwakani mjini Tabora.

Sekretarieti ya TFF iliwasilisha suala hilo kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ili itoe mwongozo kwa vile uamuzi huo uliofanywa na TPLB hauwezi kukatiwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za ligi husika.

Kamati imesisitiza kuwa hiyo ni falsafa ya mpira wa miguu ambapo uamuzi unaofanywa uwanjani haukatiwi rufani, hivyo uheshimiwe kama ilivyo kwa masuala ya mpira wa miguu kutopelekwa katika mahakama za kawaida za kisheria.

PAN AFRICAN WATAKIWA KUFUATA NGAZI HUSIKA
Wanachama wa Pan African wametakiwa kufuata ngazi husika pale wanapoona viongozi wa klabu yao wanakwenda kinyume na Katiba yao.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imetoa mwongozo huo kwa wanachama wa Pan African baada ya kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kulalamikia uongozi wao wakati wao si wanachama wa TFF.

Wanachama hao wanalalamikia uongozi wa klabu yao kwa kuitisha mkutano wa uchaguzi kabla ya ule wa kawaida ambao unatakiwa kufanyika mara moja kwa mwaka.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imelazimika kutoa mwongozo huo kwa vile wanachama hao katika malalamiko yao wamekigusa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) ambacho ni mwanachama wa TFF.

Pan African ni mwanachama wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ilala (IDFA) ambao ndiyo wanachama wa DRFA. Hivyo, TFF imemtaka mwanachama wake DRFA kupitia IDFA kufuatilia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.


Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu.

Thursday, December 26, 2013

MECHI YA MAJARIBIO TIKETI ZA ELEKTRONIKI SAA 10.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 26, 2013


Mechi ya kujaribu matumizi ya tiketi za elektroniki kati ya Azam na Ruvu Shooting inachezwa leo (Desemba 26 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo ya majaribio ni sh. 1,000 na sh. 2,000 ambapo tiketi zinapatikana kupitia M-Pesa na mawakala wa CRDB Fahari Huduma. Tiketi zitaendelea kuuzwa hadi kitakapoanza kipindi cha pili.

Mawakala 18 wa Fahari Huduma wanaouza tiketi hizo ni ABC Computer- Mtaa wa Samora, Abraham Anangisye Mwampetele- Maji Matitu, Apex Security Services- Mtaa wa Mibega, Kinyerezi, Athuman Fakhi Adam- Kongowe Mbagala, Fedha Investment Limited- Pamba Road na Fuya Godwin Kimbita- Tegeta Block.

Ghomme Health & Education Limited-Bahari Beach, Herman Arbogast Tarimo- Kigamboni, K- Finance Limited- Shekilango, Sinza, Koli Finance Limited- Mtaa wa Samora, LB Pharmacy- Mtoni Kijichi, Lista Phares Barnabas- Tabata Segerea na Maly Investment Company Limited.

Wengine ni Micu Enterprises- Mtaa wa Congo, Kariakoo, S&D Collection Company Limited- Mikocheni, Shoppers Plaza, Therry Investment Limited- Tegeta Kibaoni, TSHS Distributors Limited- Mtoni kwa Aziz Ali na Wemerick Independent Vehicle- Mtaa wa Boko, .

Mechi nyingine ya majaribio itakuwa kati ya Ashanti United na JKT Ruvu ambayo itachezwa Januari Mosi mwakani kwenye uwanja huo huo.


Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Wednesday, December 18, 2013

TANZANITE YAWASILI JOHANNESBURG KUIVAA BATSESANA.


 
Kikosi cha wachezaji 20 na viongozi tisa cha timu ya Tanzania ya wasichana chini ya miaka 20 (Tanzanite) kimewasili leo jijini Johannesburg tayari kwa mechi dhidi ya wenyeji Afrika Kusini (Batsesana).

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani nchini Canada.

Tanzanite imefikia Millpark Garden Court Hotel tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, Johannesburg kuanzia saa 9.30 alasiri kwa saa za Afrika Kusini.

Wachezaji wa Tanzanite walioko katika kikosi hicho ni Amina Bilali, Amina Hemed, Amisa Hussein, Anastaz Katunzi, Anna Mwaisula, Belina Nyamwihula, Donisia Minja, Fatuma Maonyo, Happiness Mwaipaja, Latifa Salum, Maimuna Kaimu, Najiat Idrisa, Neema Kiniga, Rehema Rhamia, Sada Hussein, Shelda Mafuru, Stumai Athuman, Tatu Salum, Theresa Kashilim na Vumilia Maarifa.

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF.

KIINGILIO MECHI YA MTANI JEMBE 5,000/-


Kiingilio cha chini kwenye mechi ya Mtani Jembe kati ya Simba na Yanga itakayochezwa Jumamosi (Desemba 21 mwaka huu) ni sh. 5,000. Kiingilio hicho ni kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648.


Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu kiingilio ni sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000, VIP C kiingilio ni sh. 15,000, VIP B itakuwa sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tu tiketi moja itapatikana kwa sh. 40,000. 



Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja katika vituo mbalimbali, mchezo huo utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.



Vituo ambavyo tiketi hizo zitauzwa keshokutwa (Ijumaa) ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.



Mechi hiyo itachezeshwa na Ramadhan Ibada (Kibo) kutoka Zanzibar, ambapo atasaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba, na Simon Charles kutoka Dodoma. Mwamuzi wa akiba ni Israel Nkongo wa Dar es Salaam wakati mtathimini wa waamuzi ni Soud Abdi wa Arusha.

Friday, December 13, 2013

FA MIKOA YAPATA MIPIRA TFF




Desemba 13, 2013

                                          
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa mipira kumi kwa kila chama cha mpira wa miguu cha mkoa ili isaidie kuendesha ligi za mikoa husika.



Mipira hiyo 250 yenye thamani ya sh. 16,250,000 tayari imeanza kutumwa kwa makatibu wa vyama vya mikoa husika. Mpira mmoja una thamani y ash. 65,000.



Ni maratajio ya TFF kuwa mipira hiyo itakuwa chachu kwa vyama vya mikoa katika uendeshaji wa ligi hizo.



MITIHANI YA WAAMUZI KUFANYIKA JUMAPILI

Robo ya mwisho ya mitihani ya waamuzi (Cooper Test) na utimamu wa mwili (physical fitness test) kwa mwaka 2013 kwa waamuzi inafanyika Jumapili (Desemba 15 mwaka huu).



Mitihani hiyo inayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam inashirikisha waamuzi wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (TFF) na wale wa kundi la waamuzi (elite) ambao wanaweza kupendekezwa kupewa beji za FIFA.



Wakufunzi wa mitihani hiyo ya waamuzi ni Leslie Liunda, Soud Abdi na Riziki Majala.



Waamuzi wa FIFA watakaofanya mitihani hiyo ni Ferdinand Chacha, Hamis Chang’walu, Israel Mujuni, Jesse Erasmus, John Kanyenye, Josephat Bulali, Mgaza Kinduli, Oden Mbaga, Ramadhan Ibada, Samwel Mpenzu na Waziri Sheha.



Washiriki kutoka kundi la elite ni Charles Simon, Dalali Jaffari, Hellen Mduma, Issa Bulali, Issa Vuai, Janeth Balama, Jonesia Rukyaa, Judith Gamba, Lulu Mushi, Martin Saanya, Mfaume Nassoro na Mohamed Mkono.



KILIMANJARO STARS YAREJEA DAR

Timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) iliyoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika jana jijini Nairobi, Kenya inarejea jijini Dar es Salaam leo.



Kilimanjaro Stars iliyomaliza michuano hiyo katika nafasi ya nne inatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 12 kamili jilioni kwa ndege ya RwandAir.



Wenyeji Kenya (Harambee Stars) ndiyo walioibuka mabingwa wa michuano hiyo baada ya kuifunga Sudan mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa jana Uwanja wa Nyayo.

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF

Sunday, December 8, 2013

ZAMBIA NA SUDANI ZATINGA NUSU FAINALI MICHUANO YA CHALLENGE.



Timu za taifa za Zambia Chipolopolo na Sudani zimefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya kombe la Challenge inayoendelea huko nchini Kenya kwakushirikisha mataifa wanachama wa Cecafa.
Katika michezo ya robo fainali iliyochezwa leo kwenye mashindano hayo timu ya taifa ya Sudani imefanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kuifunga Ethiopia magoli 2 kwa 0.
Katika mchezo wa awali hii leo Zambia iliitoa Burundi kwa changamoto ya Penalti baada ya kuifunga penalty 4 kwa 3 hii ikiwa ni baada ya kutoka suluhu ya kutofungana katika muda wa dakika 90.
Kwamatokeo hayo Zambia na Sudani zinaungana na Kilimanjaro Stars pamoja na wenyeji Kenya kutinga hatua hiyo mhimu ambayo itategua kitendawili cha nani na nani wataingia fainali.

RAIS KIKWETE ATOA CHANGAMOTO KWA TFF JUU YA MAENDELEO YA SOKA NCHINI.



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mh  Jakaya Mrisho Kikwete ametoa changamoto kwa uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusukuma mbele zaidi gurudumu la maendeleo ya mchezo huo.

Rais ametoa changamoto hiyo katika barua yake kwa Rais mstaafu wa TFF, Leodegar Tenga na kumtaka asichoke kutoa ushauri na uzoefu wake kila utakapohitajika katika shughuli mbalimbali zinazohusu maendeleo ya mpira wa miguu hapa nchini Tanzania.

Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo wakati akijibu barua ya Tenga iliyokuwa ikimuarifu kuhusu kumaliza kipindi chao cha uongozi, na kumshukuru yeye binafsi (Rais Kikwete) na Serikali anayoiongoza kwa mchango waliotoa katika kuendeleza mpira wa miguu nchini.

“Pongezi zako zimetupa moyo na ari ya kuongeza maradufu juhudi zetu za kuboresha kiwango cha ubora wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.
“Kwa niaba ya Serikali napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwako wewe na uongozi wote uliopita wa TFF kwa mchango wenu muhimu mlioutoa wa kuendeleza mpira wa miguu nchini.
“Mafanikio ya kutia moyo yamepatikana chini ya uongozi wako,” amesema Rais Kikwete katika barua yake hiyo na kumtakia kila la heri Tenga katika shughuli zake.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Tanzania bado haijafika pale ambapo inapataka, lakini dalili njema zimeanza kuonekana, hivyo kinachotakiwa sasa ni uongozi mpya kusukuma mbele zaidi gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu nchini.
Tenga ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) aliiongoza TFF kwa vipindi viwili kuanzia Desemba 2004 hadi Oktoba 2013.